🌠Languages
SMZ Logo

SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA ZANZIBAR

ZDCEA Logo
Habari mpya

Wanne Kizimbani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya
image
Imewekwa: 13/07/2026

VIJANA wanne, akiwemo raia wa Romania, Alexandru Rizescu, wamefikishwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, Tunguu, wakikabiliwa na makosa mbalimbali yanayohusiana na usafirishaji, uhifadhi na uuzaji wa dawa za kulevya.
Watuhumiwa wengine ni Ali Saiid Abdalla (52) mkazi wa Amani,Feisal Masoud Said (31) mkazi wa Vikokotoni na Mussa Burhan Msoma (49) mkazi wa Kisauni.
Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani mbele ya Jaji Said Hassan Said, ambapo walisomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),Ayoub Nassor Sharif.
Akisoma hati ya mashitaka, wakili huyo alidai kuwa Alexandru Rizescu na Ali Saiid Abdalla walitenda kosa la kusafirisha dawa za kulevya kati ya mwezi Desemba mwaka jana na Januari 6 mwaka huu katika Bandari ya Malindi, Zanzibar.
Ilidaiwa kuwa watuhumiwa hao waliingiza nchini kutoka China, kupitia usafiri wa majini unaomilikiwa na kampuni ya Slim Trading Limited, viboksi 132 vya shisha vyenye maandishi ya Elfbar. Ndani ya viboksi hivyo kulikutwa viambata vya dawa za kulevya aina ya cocaine vyenye uzito wa gramu 750.069.
Mahakama ilielezwa kuwa kitendo hicho ni kosa chini ya sheria za udhibiti wa dawa za kulevya.
Aidha, upande wa mashitaka ulidai kuwa siku hiyo hiyo watuhumiwa hao walisafirisha viboksi 220 vilivyokuwa na viambata vya dawa za kulevya aina ya Lysergic Acid Diethylamide (LSD) vyenye uzito wa gramu 996.358.
Katika shtaka jingine, Alexandru Rizescu, Ali Saiid Abdalla na Feisal Masoud Said wanadaiwa kuuza dawa za kulevya Januari 26 mwaka huu majira ya saa 7:30 mchana katika eneo la Shangani, Wilaya ya Mjini, Unguja.
Ilidaiwa kuwa ndani ya duka la ‘’SHOP ‘N’ GO’’, watuhumiwa hao walikuwa wakiuza bidhaa za shisha zilizokuwa zimechanganywa na dawa za kulevya aina ya cocaine yenye uzito wa gramu 750.
Upande wa mashitaka pia ulidai kuwa watuhumiwa hao walikutwa na mashine 49 zinazodaiwa kutumika kusagia na kuandaa dawa za kulevya, jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria.
Katika shtaka lingine, watuhumiwa hao pamoja na Mussa Burhan Msoma wanadaiwa kuwa Januari 29 mwaka huu majira ya saa 7:30 mchana katika eneo la Mpendae, walikutwa wamehifadhi vipisi 560 vya shisha vilivyokuwa na viambata vya dawa za kulevya aina ya Lysergic Acid Diethylamide (LSD) ndani ya ghala lililopo Mpendae.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, watuhumiwa wote walirudishwa rumande hadi Novemba 10 mwaka huu, ambapo kesi hiyo itaanza kusikilizwa kwa ushahidi.