🌠Languages
SMZ Logo

SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA ZANZIBAR

ZDCEA Logo
Habari mpya

image
Wanne Kizimbani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya

VIJANA wanne, akiwemo raia wa Romania, Alexandru Rizescu, wamefikishwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar, Tunguu, wakikabiliwa na makosa mbalimbali yanayohusiana na usafirishaji, uhifadhi na uuzaji wa dawa za kulevya.
Watuhumiwa wengine ni Ali Saiid Abdalla (52) mkazi wa Amani,Feisal Masoud Said (31) mkazi wa Vikokotoni na Mussa Burhan Msoma (49) mkazi wa Kisauni.
Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani mbele ya Jaji Said Hassan Said, ambapo walisomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),Ayoub Nassor Sharif.
Akisoma hati ya mashitaka, wakili huyo alidai kuwa Alexandru Rizescu na Ali Saiid Abdalla walitenda kosa la kusafirisha dawa za kulevya kati ya mwezi Desemba mwaka jana na Januari 6 mwaka huu katika Bandari ya Malindi, Zanzibar.
Ilidaiwa kuwa watuhumiwa hao waliingiza nchini kutoka China, kupitia usafiri wa majini unaomilikiwa na kampuni ya Slim Trading Limited, viboksi 132 vya shisha vyenye maandishi ya Elfbar. Ndani ya viboksi hivyo kulikutwa viambata vya dawa za kulevya aina ya cocaine vyenye uzito wa gramu 750.069.
Mahakama ilielezwa kuwa kitendo hicho ni kosa chini ya sheria za udhibiti wa dawa za kulevya.
Aidha, upande wa mashitaka ulidai kuwa siku hiyo hiyo watuhumiwa hao walisafirisha viboksi 220 vilivyokuwa na viambata vya dawa za kulevya aina ya Lysergic Acid Diethylamide (LSD) vyenye uzito wa gramu 996.358.
Katika shtaka jingine, Alexandru Rizescu, Ali Saiid Abdalla na Feisal Masoud Said wanadaiwa kuuza dawa za kulevya Januari 26 mwaka huu majira ya saa 7:30 mchana katika eneo la Shangani, Wilaya ya Mjini, Unguja.
Ilidaiwa kuwa ndani ya duka la ‘’SHOP ‘N’ GO’’, watuhumiwa hao walikuwa wakiuza bidhaa za shisha zilizokuwa zimechanganywa na dawa za kulevya aina ya cocaine yenye uzito wa gramu 750.
Upande wa mashitaka pia ulidai kuwa watuhumiwa hao walikutwa na mashine 49 zinazodaiwa kutumika kusagia na kuandaa dawa za kulevya, jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria.
Katika shtaka lingine, watuhumiwa hao pamoja na Mussa Burhan Msoma wanadaiwa kuwa Januari 29 mwaka huu majira ya saa 7:30 mchana katika eneo la Mpendae, walikutwa wamehifadhi vipisi 560 vya shisha vilivyokuwa na viambata vya dawa za kulevya aina ya Lysergic Acid Diethylamide (LSD) ndani ya ghala lililopo Mpendae.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, watuhumiwa wote walirudishwa rumande hadi Novemba 10 mwaka huu, ambapo kesi hiyo itaanza kusikilizwa kwa ushahidi.


2026-07-13

image
ZDCEA NA DCEA ZAADHIMISHA SIKU YA KUPIGA VITA MATUMIZI NA BIASHARA HARAMU YA DAWA ZA KULEVYA DUNIANI.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekua ikichukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na uhalifu wa dawa za kulevya sambamba na kuanzisha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na dawa hizo nchini.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt Hussein Ali Mwinyi katika maadhimisho ya kilele cha siku ya kupiga vita matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya duniani hafla iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya tume ya uchaguzi Maisara wilaya ya mjini unguja.

Amesema kuwa Zanzibar ikiwa nisehemu ya Dunia inaungana na Mataifa mengine katika kuadhimisha siku hii hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kutambua kuwa matumizi ya dawa za kulevya ni tatizo linaloendelea kuyasumbua Mataifa yote duniani hususan vijana katika kila pembe ya dunia wanaendelea kujiingiza katika janga hili baya siku hadi siku.

Makamu wa pili wa rais wa Zanzibar amesema serikali imejipanga Kusambaratisha mitandao ya wahalifu wakubwa wa dawa za kulevya pamoja kutaifisha mali mbali mbali za wahusika wa dawa hizo wa ndani na nje ya nchi.

Mhe. Hemed amesema Serikali imeimarisha huduma za tiba na marekebisho ya tabia kwa kujenga vituo vya kutoa huduma kwa waathirika lakini bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo, Mabadiliko ya mara kwa mara ya mbinu zinazotumiwa na wahalifu ikiwemo utengenezaji wa dawa mpya za kulevya zenye muundo tofauti na dawa za asili kama vile bangi, cocaine na heroine na zenye athari zaidi ya dawa za kulevya katika pipi, chocolate, biskuti na sigara za kiektroniki pamoja na Matumizi ya teknolojia katika biashara hiyo haramu pamoja na kuongezeka ushawishi kwa vijana kupitia mitandao ya kijamii.

Sambamba na hayo mhe hemed ametoa wito kwa wazazi, walezi, viongozi wa dini, walimu na jamii kwa ujumla kuendelea kusimamia malezi bora ya vijana pamoja na kuzikumbusha familia ambazo ndio msingi wa kwanza wa wa kinga dhidi ya dawa za kulevya, kuongeza juhudi za kuwekeza kwenye maadili, elimu na mawasiliano mazuri ndani ya familia kwani bila ya kufanya hivyo taifa litakosa nguvu kazi ya baadae.

Aidha, ameviagiza vyombo vinavyohusika na mapambano dhidi ya dawa ya kulevya kushirikiana na Mamlaka husika katika kuwafichua wahalifu wa dawa za kulevya na kuacha muhali. 

2026-07-22